![]() |
Marehemu Levina Mmasi akilishwa chakula na aliyetarajia kumuoa, Kasisi Masawe kwenye hafla ya kuagwa kwake (Send-Off Party) iliyofanyika Jumatano iliyopita. |
Tanga, Handeni. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Bibi
Harusi ambaye ni mkazi wa Chanika mjini Handeni, Levina Mmasi (23)
amefariki dunia saa moja kabla ya ndoa yake kufungwa katika Kanisa la
Katoliki la Roma Wilaya Handeni Jumamosi na hivyo kuilazimu kamati ya
maandalizi ya harusi kujigeuza na kuwa ya msiba.
Kifo hicho kilichotokea Jumamosi mwishoni mwa wiki
iliyopita, kimekuwa gumzo mjini Handeni huku wananchi wakisema kuwa ni
tukio ambalo halijawahi kutokea katika wilaya hiyo.
Msemaji wa familia ya marehemu aliyejitambulisha
kwa jina la Firmin Mrimasha, alisema kuwa chanzo cha kifo cha Levina
ambaye alijifungua mwanzoni mwa wiki iliyopita,ilikuwa ni homa
aliyoipata ghafla siku ya Alhamisi na kupelekwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Handeni na kukutwa na malaria na kisha kulazwa kwa matibu.
“Huyu bibi harusi alikuwa ametoka kujifungua,
alikuwa na mtoto wa kiume kutokana na ujauzito wa miezi saba, ndipo
ghafla Alhamisi akapata homa tukampeleka hospitali alikolazwa na baada
ya kupata nafuu, aliruhusiwa Ijumaa.
“Baada ya kuruhusiwa akaanza maandalizi ya harusi
na Jumamosi ambayo ndiyo siku ya ndoa yake, alijiandaa lakini ilipofika
saa 8.05 akafariki dunia akiwa nyumbani akisubiriwa kwenda kanisani
kufunga ndoa ambayo ilikuwa ifungwe saa 9.00,” alisema Mrimasha.
Alisema, “Inasikitisha sana ila imeshatokea yaani
marehemu amefariki saa moja kabla ya ndoa yake na baada ya kifo hicho,
mtoto wake naye alifariki muda mfupi baada ya mama yake kufariki dunia,”
alisema Mrimasha.
Akizungumzia mkasa huo, Mwenyekiti wa Kamati ya
Harusi hiyo iliyogharimu Sh7.7 milioni, Abdi Kipacha alisema kuwa kwake
ni tukio la kwanza kutokea tangu kuzaliwa kwake na kamwe hawezi
kulisahau.
“Nilishazipangia kazi kamati za maandalizi, lakini
ghafla tukapewa taarifa kuwa bibi harusi amefariki...Hatukuamini,
ikabidi niwatangazie wanakamati wenzangu kuwa hakuna tena shughuli, bibi
harusi amefariki,” alisema mwenyekiti huyo wa kamati na kuongeza:
“Kitu tulichokuwa tukisubiri ni kuambiwa bibi
harusi angefika saa ngapi, lakini ghafla tukapewa taarifa za kifo,
ilikuwa ni vigumu kuamini lakini ni kweli imetokea na inasikitisha kwani
si jambo la kawaida,” alisema Kipacha.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wanandugu ni
kuwa marehemu alikuwa Mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi na
kwamba alikuwa katika kundi la walimu wa ajira mpya ambayo hadi mauti
yanamkuta alikuwa hajapokea hata mshahara wake wa awali.
Akizungumzia hali hiyo, Padri aliyekuwa afungishe
ndoa hiyo, Max Sabuni wa kanisa hilo Katoliki Handeni alisema:
“Nimesikitishwa na tukio hili kwa kuwa halikuwahi
kunitokea...Kilichobaki ni wanandugu kuwa watulivu kwa kuwa Mungu
amechukua kiumbe wake kwa muda alioupanga.”
Aliwataka ndugu, jamaa na marafiki kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi.
Naye mume wa marehemu, Kasisi Masawe alisema:
“Nimechanganyikiwa sana na hili...Ni jambo ambalo sikulitarajia.
Ninamshukuru Mungu kwa yote japokuwa kifo hiki kimeniharibia mipango
yangu mingi ya maisha na Levina.
“Nilipanga mengi na yeye, lakini Mungu
hakupenda...Nilimpenda sana Levina,leo ameniacha. Amekwenda na
mwanangu...Ni pigo kubwa kwa kweli, mke na mtoto kwa wakati mmoja,
inauma sana.”
Mwili wa bibi harusi huyo ulisafirishwa jana
kupelekwa Machame mkoani Kilimanjaro kwa maziko ambayo yanafanyika leo
Jumatano pamoja na mtoto wake ambaye naye alifariki saa chache baada ya
mama yake.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine
Massawe alithibitisha kutokea tukio hilo lakini akasema hawezi
kuzungumzia kwa undani kwa kuwa ni tukio la kifamilia zaidi.
No comments:
Post a Comment