Mifuko ya plastiki inayofungasha pombe maarufu kama ‘viroba’ imepigwa marufuku na Serikali kuanzia mwakani.
Sambamba na hilo Serikali pia, imepiga marufuku moja kwa moja utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki kuanzia mwaka huo.
Sambamba na hilo Serikali pia, imepiga marufuku moja kwa moja utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki kuanzia mwaka huo.
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliwaambia wanahabari jana sehemu kubwa ya mifuko hiyo inayotolewa bure imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa.
Wakati Makamba akiyasema hayo, Februari mwaka huu Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina aliondoa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki akisema kuwa itaziweka rehani ajira za Watanzania wanaofanya kazi kwenye viwanda vinavyotengeneza mifuko hiyo.
Pia, Mpina alisema itapunguza kasi ya uwekezaji wa viwanda vilivyowekeza katika bidhaa hiyo.
Akizungumza katika siku ya Mazingira Afrika, Mkurugenzi wa Mazingira, Dk Julius Ningu alisema maamuzi hayo yamelenga kulinda viwanda vilivyoajiri mamia ya Watanzania, tofauti na nchi nyingine zinazotegemea wazalishaji wa nje ya nchi.
Makamba akizungumzia uamuzi mpya wa kuzuia mifuko ya plastiki, alisema matumizi ya mifuko inayofungashia vileo na inayotumika katika matumizi mengine husambaa na kuchafua mazingira. Alisema mifuko ya plastiki inatajwa kuziba mifereji na kusababisha mafuriko na athari nyingine za mazingira.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema Serikali inakamilisha majadiliano ya ndani na baadaye itawahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku ya moja kwa moja mifuko hiyo.
Alifafanua kwamba Serikali itatoa muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko hiyo ili kujiandaa kuacha shughuli hizo na badala yake itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikanaji wa vifungashio mbadala.

Aliongeza kuwa katika kuonyesha Serikali imedhamiria kupambana na hali hiyo wizara yake imeamua kutuma timu ya watu watano kwenda Rwanda kujifunza namna bora ya kudhibiti matumizi na kuzuia mifuko hiyo tangu mwaka 2008.
Waziri huyo alitoa wito kwa watengenezaji, wasambazaji na waagizaji wa mifuko hiyo kujiandaa na zuio hilo na katika siku zijazo Serikali itatoa utaratibu na maelekezo ya tarehe ya kuanza zuio huku taratibu nyingine za kina zikifuata ili kuondoa mkanganyiko.
Katika hatua nyingine, Makamba alisema maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka hayatafanyika kitaifa badala yake wizara imewaelekeza wakuu wa mikoa kufanya maadhimisho katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Makamba, kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa juu ya maadhimisho hayo ni ‘ tuhifadhi vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu’aliwashauri na kuwataka Watanzania kutumia siku hiyo kupanda miti, kudhibiti uchomaji wa misitu .
MWISHO:
No comments:
Post a Comment