Nafahamika kwa jina Bahati Anthony ambaye ni fundi nguo maarufu, amenusurika na kifo baada ya kunaswa na watu wenye hasira kali kwa kutaka kumtapeli wakala wa mitandao ya simu inayotoa huduma ya kuweka na kutoa fedha M - PESA.
Tukio hilo limetokea maeneo ya Masika katikati ya Mji wa Morogoro kwenye duka la wakala aitwaye Gelasi Assenga ambapo jamaa huyo alijikuta akiloa damu chapachapa.
Akisimulia tukio hilo, Assenga amesema “Jana huyu jamaa alikuja hapa akatuma shilingi 15, leo amekuja ameniambia nitume laki tatu kwenye namba ileile aliyonipa jana.
“Baada ya kutuma, nimemwambia anipe hiyo laki tatu anadai yeye ni wakala wa Freemason hivyo baada ya dakika 10, begi alilobeba litajaa fedha na atanilipa. Nimesubiri dakika 10 zimepita.
“Nimemwambia anipe fedha zangu, anasema haijaingia, nikaamua kumpekua kwenye begi nikakuta mshumaa.”
“Wakati napekuwa ndipo akaanza kukimbia. Nilipoona nitapoteza fedha zangu, nikaona nimwitie mwizi ndipo watu wakamkamata na kumshushia kichapo.
Nilipoona wanataka kumuua, nilikodi bodaboda na kumpeleka polisi ambako aliamuriwa kurudisha fedha zangu ambapo aliwapigia simu ndugu zake kutoka Kigoma ambao walidai kuwa watanitumia fedha yangu ndipo aachiwe huru.”
Kwa upande wake, fundi huyo amesema “Nilisoma mabango ya Freemason yaliyozagaa mitaani yakihamasisha watu kujiunga, nilichukua namba za simu na kuwapigia ambapo waliniambia ili niwe tajiri natakiwa niwatumie shilingi elfu 15, nikatuma.
“Baadaye waliniambia ninunue begi jipya ndani yake niweke mshumaa na udi kisha niende palepale kwa wakala wa jana yake niwatumie shilingi laki tatu. “Niliwaambia fedha hiyo sina, wakaniambia nimwambie wakala anitumie tu baada ya dakika 10 begi langu litajaa fedha lakini haikuwa hivyo ndiyo maana Assenga akaniitia mwizi nikapigwa.”
MWISHO:
No comments:
Post a Comment