Sunday, June 19, 2016

MOROGORO: WATU WATATU WAFARIKI DUNIA BAADA YA KULA MIHOGO INAYOSADIKIWA KUWA NA SUMU

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro  Ulrich Mtei akizungumza na Waandishi wa Habari ambao hawako Pichani


Watu watatu  wamefariki Dunia na wengine wawili kujikuta katika hali mbaya, mara  baada ya kudaiwa kula mihogo  inayodhaniwa kuwa na sumu, katika kijiji cha Kauzeni  kilichopo kata ya Mzinga Manispaa ya Morogoro huku kati yao,  wawili wakiwa ni ndugu wa familia moja.

Tukio hilo limetokea wakati watu hao wakiwa wanajiandaa kuanza  kutengeza matofali, na ndipo walichemsha mihogo hiyo na kula, na baada ya muda mfupi hali zao zilibadilika na kukimbizwa katika hospitali ya Jeshi ya Mzinga, hata hivyo walihamishiwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro baada ya hali zao kuwa mbaya zaidi..


Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Ulrich Mtei, amesema jeshi la Polisi Mkoani humo linaendelea na uchunguzi, kujua sumu hiyo iliweka kwenye chakula hicho au ilikuwa kwenye mihogo, huku akisema  kati ya marehemu waliofariki dunia, wawili ni ndugu wa familia moja ambao ni mapacha waliojulikana kwa majina ya Omary Issa Mohamed na Hamis Issa Mohamedi huku mwingine akijulikana kwa jina la Wakusizi.
.
                    Mmojawapo Aliyenusurika katika tukio hilo Anaitwa Joshua Msiani
Kamanda Mtei amesema miili ya Marehemu watatu waliofariki kutokana na kula mihogo  hiyo yenye sumu, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospital ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kusubili taratibu za mazishi kutoka kwa ndugu wa marehemu.

Hatua nyingine mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Jackson John ambaye inasadikiwa ni mgonjwa wa akili, amemuua ndugu yake  wa damu (Mdogo wake) aitwaye Raymond Meckioli (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa wa Pili, katika  shule ya Msingi Kikeo, wilayani Mvomero, kwa kumchoma na mkuki  tumboni, kisha na yeye kujiua kwa kutumia mkuki huo huo, kwa kujichoma sehemu ya ubavuni.

MWISHO:




No comments:

Post a Comment