Monday, May 30, 2016

NAMUNGO FC KUTOKA LINDI WAONGOZA LIGI YA MABINGWA WA MIKOA KITUO CHA MOROGORO

Mchezaji wa Namungo FC Kutoka Lindi Emmanuel Thomas akijaribu kumtoka Beki wa Timu ya Sifa United ya Jijini Dar es salaam

Timu ya Namungo FC kutoka Lindi Jimbo la Ruangwa ambalo mbunge wake ni waziri Mkuu Kasim Majaliwa  imeendelea kujisafishia njia ya kupanda ligi daraja la Pili baada ya jana kuinyuka timu ya Sifa Poltani ya Temeke Dar es salaam kwa  bao 2-1 kwenye fainali za ligi ya Mabingwa wa Mikoa kituo cha Morogoro inayoendele katika uwanja wa Jamhuri.

Kwa ushindi huo Namungo FC inayolelewa na Waziri Mkuu Majaliwa inaongoza kituo hicho kwa kujikusanyia alama 7 wakiwa wamecheza michezo mitatu huku Stendi ya Singida iliyopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye ligi hiyo ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na alama 3 huku ikicheza   michezo miwili.

Katika mchezo wa jana uliokuwa mkali kwa muda wote wa dakika 90 Namungo ambayo pia inamilikiwa na wachimba madini wa Namungo ilijipatia bao la kwanza dakika 11 kupitia kwa Yahaya Hamis na goli la pili likifungwa dakika 38 kupita kwa Emmanuel Thomas .

 Bao la kufutia machozi la Sifa lilifungwa  na Marick Dege kwa mkwaju wa penati  dakika 73 baada ya beki mmoja wa Namungo FC kumkwatua Hamis na Mwamuzi Mohamed Thofiri'Kolina' aliamuru ipigwe penati.

Kivumbi hicho kianatarajiwa kuendelea leo katika uwanja wa jamhuri pale timu nne zitakaposhuka dimbani kupambana, Mchezo wa kwanza unaotarajiwa kuanza saa nane mchana utawakutanisha  timu ya Stand FC ya Pwani dhidi ya timu ya Muheza United ya Mkoani Tanga. Mchezo wa pili unaotarajiwa kuanza saa kumi jioni ni baina ya timu ya Mbuga FC kutoka mkoani Mtwara dhidi ya timu ya Stand Misuna  ya Singida.

MWISHO:
 
 



















No comments:

Post a Comment