Tuesday, May 31, 2016

WACHEZAJI WA MUHEZA UNITED KUTOKA TANGA WAUGUA KIPINDUPINDU, WAKIMBIZWA HOSPITALI YA SABASABA MOROGORO


Timu ya soka ya Muheza United FC ya mkoani Tanga imeshindwa kuendelea na michezo ya ligi ya mabingwa ya mikoa kati ya wapinzania wao baada ya wachezaji 11 kuugua ghafla ugonjwa wa kipindupindu na kulazwa katika kituo cha afya cha Sabsaba Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza na muandishi wa habari hii, Msimamizi wa kituo cha Morogoro kutoka TFF, Charles Ndagala amesema kuwa mchezo kati ya Stend FC ya Pwani na Muheza United FC uliotakiwa kufanyika tarehe 30 May 2016 saa nane  mchana umesogezwa mbele kufuatia wachezaji 11 wa Muheza United kuugua ugonjwa wa kipindupindu. 

Ndagala alisema kutokana na dharura hiyo mchezo huo utapangwa siku nyingine hadi hali ya wachezaji hao watapotengemaa afya zao.

“Mgonjwa wa kwanza aligundulika majira ya saa 8 usiku na wengine wanne kukimbizwa hospitali ya mkoa wa Morogoro ambapo walipimwa na kugundulika kuwa wanaugua ugonjwa wa kipindupinduu.”amesema Ndagala.

Baada ya kugundulika kuugua kipindupindu wagonjwa wengine walikimbizwa moja kwa moja kituo cha afya Sabasaba.

Kocha mkuu wa timu ya soka ya Muheza United FC, John King Kibwana aliwataja wachezaji hao waliolazwa katika kituo cha Afya Sabasaba Manispaa ya Morogoro kuwa ni pamoja na Iddi Bohero, Ramadhan Rajabu, Jerd Stephen, Nirmo Rashid Sendeka, Abdul Mashaka, Pima Omari, Athuman Mwandani, Robert Newa, Iddi Kadabla na Iddi Ramadhani.

Afisa afya wa Manispaa ya Morogoro Dkt Gabriel Malissa alisema kuwa walipokea wagonjwa 11 na wamelazwa katika kituo cha afya Sabasaba na hali zao zinaendelea vizuri.


MWISHO:

No comments:

Post a Comment