
MAUAJI ya Watanzania kwa njia ya kuchinjwa yanaendelea kushika kasi baada ya usiku wa kuamkia jana wakazi wanane wa kitongoji cha Kibatini, kata ya Mzizima jijini Tanga kukusanywa kwa mwenyekiti wa kitongoji na kisha kuuawa kwa kuchinjwa shingo na watu wasiojulikana.
Watu hao ambao inadaiwa kuwa ni majambazi walivamia usiku wa kuamkia jana kwa kuvunja milango ya nyumba tatu ambazo wakazi hao walikuwa wamelala na kuwachinja kisha kuiba biskuti, mchele na sukari na kutokomea navyo kusikojulikana.
Wauaji hao inadaiwa wana uhusiano na wahalifu ambao wamekuwa wakijificha ndani ya mapango ya Majimoto na kujihusisha na matukio kadhaa ya uvamizi ili kupora vyakula na kusababisha mauaji ya wakazi wa Jiji la Tanga, ikiwamo katika duka kuu la Central Bakery mwishoni mwa Aprili mwaka huu.
Mmoja wa shuhuda wa mauaji hayo, Kea Leonard (70) ambaye pia ni mkazi wa Kibatini, katika mahojiano jana alisema wanaamini kwamba chanzo cha mauaji ya wenzao ni kulipiza kisasi.
“Wiki iliyopita majira ya saa tano asubuhi hapa tulikamata vijana saba kati ya wanane wenye umri wa kama miaka 13 ambao walikuwa wakiranda randa hapa kitongojini ili kutafuta namna ya kuvuka mto kwenda ng’ambo ya pili na ndipo mmoja wao alipotutoroka,” alieleza Leonard
Aliongeza kwamba wakati wahalifu hao wanavamia nyumba ya mjumbe wa serikali ya kitongoji kabla ya kumtoa nje walisikia mmoja wa watu hao akimhoji kuhusu mahali walipopelekwa watoto saba.
Diwani wa Kata ya Mzizima, Fredrick Charles alizungumza na waandishi wa habari na kuthibitisha kwamba kati ya watu waliokufa mmoja ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mleni uliopo kwenye kata hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul alithibitisha mauaji hayo. “Mei 30, mwaka huu majambazi waliokuwa na visu na mapanga walivamia kaya tatu na kuua wananchi majira ya saa saba usiku,” alisema Kamanda Paul.
Aliwataja waliouawa ni Issa Hussein (50) ambaye ni mmiliki wa kaya hiyo pamoja na kuibwa biskuti, mchele na sukari katika duka dogo. Wa kaya nyingine ni Mkola Hussein (40) na Hamis Issa (20), Hamis Issa (20) na aliyemtaja kwa jina la Mikidadi (70).
Kamanda aliwataja marehemu wengine ni Mahamud (35) ambaye ni mkwe wa Mikidadi, Issa Ramadhani (25), Kadir (25) na Salum ambao ni wachunga ng’ombe kijijini humo.
MWISHO:
No comments:
Post a Comment