
MISRI imekata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon, baada ya kuwafunga wenyeji, Tanzania mabao 2-0 jioni ya leo uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanawafanya Misri wamalize mechi za Kundi G wakiwa na pointi 10 baada ya mechi nne, wakishinda tatu na kutoa sare moja, wakati Tanzania inabaki na pointi yake moja na inashika mkia nyuma ya Nigeria yenye pointi mbili.
Hadi mapumziko, tayari Misri walikuwa mbele kwa 1-0 bao lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea ya England, Mohammed Salah dakika ya 43 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki Mwinyi Hajji Mngwali kumkwatua nje kidogo ya boksi Nagram Fahmy.
Katika kipindi hicho, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kila upande
ulipoteza nafasi za wazi huku taifa Stars wakionyesha uhai licha ya kupiga mpira ambayo ilikuwa inaishia miguuni mwa mabeki wa Misri.
Dakika ya 27, mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu aliunganishia juu ya lango krosi ya Elias Maguri na dakika ya 30, Nahodha Mbwana Ally Samatta alipewa pasi nzuri na Farid Mussa akapiga nje.
Kipindi cha pili, Taifa Stars walikianza vizuri na kufanikiwa kupata penati dakika ya 53 iliyotolewa baada ya kiungo Himid Mao kuangushwa na Ame Medhat hata hivyo, mpigaji wa penati hiyo ambaye ni Nahodha Mbwana Samatta aliweza kupaisha juu ya lango mkwaju wake.
Salah akaifungia bao la pili Misri dakika ya 58 baada ya kumpita beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali aliyecheza chini ya kiwango mno hii leo.
Kocha Charles Boniface Mkwasa akamtoa Mngwali baada ya kuchomesha
kwa mara ya pili na kumuingiza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, aliyekwenda kumalizia vizuri.
Kikosi cha Timu ya Tanzania "TAIFA STARS" Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk68, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao, Thomas Ulimwengu/Deus Kaseke dk73, Mwinyi Kazimoto, Elias Maguli/John Bocco dk62, Mbwana Samatta na Farid Mussa.
Kikosi cha Misri; Essam Kamal Tawfik, Alg Gabr Mossad, Ramy Hisham Abdel, Mohamed Abdel Sayed, Abood Abdulrahamn Amed, Tarek Hamad Hamed, Mohamed Nasser Elsayed, Mohamem Ahmed Ibrahim, Abdallah Mahamoud Said na Nagram Mohsin Fahmy.
MWISHO:
No comments:
Post a Comment