Monday, October 17, 2016

DED WA MKINGA APANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA KUMTISHIA KUMUUA NA BASTOLA ASKARI WA USALAMA BARABARANI


NA, PETER LAURENCE
Bastola ya Mkurugenzi Huyo iliyoitumia kumtishia kumuua askari wa usalama Barabarani


Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro limemfikisha mahakamani Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mkinga mkoani Tanga Emmanuel Mkumbo mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, kwa tuhuma za kumtishia  kumuua kwa  bastola askari wa usalama barabarani, wakati akiwa katika majukumu yake ya kikazi pamoja na kuvunja sheria za usalama barabarani.

Gari binafsi aliyokuwa anaitumia mkurugezi wa Halmashauri ya Mkinga

Hapa akijifichwa kupigwa picha na Waandishi wa Habari

Mtuhumiwa huyo amesomewa mashtaka mawili mbele ya hakimu Agripina Kimanze chini ya mwendesha mashtaka wa serikali Sunday Hyera pamoja na Edger Bantulaki, ambapo kosa la kwanza ni kutishia kuua na la pili ni makosa ya usalama barabarani ambayo yote amekana kuhusika nayo.

Tukio hilo limetajwa kutokea October 15 mwaka huu, katika eneo la mkambarani pembezoni kidogo mwa mji , ambapo mtuhumiwa huyo  alikuwa akiendesha gari aina Prado ya  yenye namba za usajili T 845 CTJ na aliposimamishwa na askari hao wa usalama barabani kutokana na kuendesha gari hiyo kwa mwendo kasi, akagoma kutoa ushirikiano kwa askari aliyemsimamisha na kudai yeye ni mfanyakazi wa serikali.

Baada ya kushindwa kuelewana na askari huyo, mkurunguzi huyo  aliomba kuonana na mkuu wa kituo katika eneo hilo, hata hivyo wakati akipelekwa na askari mmoja aliyefahamaika kwa jina moja la Titunda kupitia gari hilo, Mkurungezi huyo alimtolea bastola askari huyo na kumtaka kushuka kwenye gari na yeye kugeuza na kuendelea na safari yake, hata hivyo alipofika katika eneo la Mikese, aliweza kukamatwa na askari waliokuwa wamepewa taarifa juu ta tukio hilo.

Baada ya kukutwa na makosa hayo mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo,ikiwemo ya kutishia kuua, kuendesha gari bila kuwa na bima pamoja na kuendesha kwa mwendo kasi, Makosa ambayo yote ameyakana.

Mkurugenzi huyo ameachiwa kwa dhamana na kesi yake imetapangwa kusikilizwa tena Oktoba 31 ya mwaka huu.

MWISHO:




No comments:

Post a Comment