Tuesday, December 5, 2017

KESI INAYOWAKABILI WABUNGE WA CHADEMA SUZANA KIWANGA NA PETER LIJUALIKALI YAPIGWA KALENDA MPAKA DESEMBA 6 MWAKA HUU

Na, Omary Hussein, Morogoro


Mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Morogoro, kwa mara nyingine imeshindwa kutoa dhamana kwa Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Peter Lijualikali wa Kilombero pamoja na Suzani Kiwanga wa Mlimba na washtakiwa wengine 34 wa Chama hicho, baada ya kutokea mvutano wa kisheria baina ya upande  wa Mawakili wa Serikali na ule wa utetezi, juu ya kiapo kilichowasilisha na Serikali cha kupinga washtakiwa hao kupatiwa dhamana, hatua iliyopelekea Hakimu Ivan Msaki, kuhairisha tena kesi hiyo hadi Desemba 6, watakapojadili tena kiapo hicho.

Wabunge hao pamoja na washtakiwa wengine 34 wanafikishwa mahakamani hapo, wakishtakiwa kwa makosa nane ambayo ni Kula njama ya kutenda kosa, Mkusanyiko usio wa halali, Kufanya Ghasia,  uchochezi wa kutenda kosa shtaka ambalo linawakabili Mbunge Peter Lijualikali na Suzani Kiwanga, Shtaka la tano likiwa kuchoma nyumba mali ya Serikali ya Kijiji, sita Uharibifu wa mali  zenye thamani ya Milioni 100.8   huku shitaka la saba na nane likiwa ni uharibu wa mali kwa makusudi, Makosa ambayo wanadaiwa kuyatenda  Novemba 26 , mwaka huu katika kata ya Sofi Wilayani Malinyi kwenye uchaguzi mdogo wa marudio ya Udiwani.

Awali upande wa mawakili wa Serikali, unaoongozwa na Sunday Hyera kwa kushirikiana na Edgar Bantulaki waliwasilisha kiapo cha kupinga dhamana kwa washtakiwa hao, upande wa utetezi wa washtakiwa, unaoongozwa na Wakili Barthalomeo Tarimo pamoja na Peter Kibatala, uliiomba mahakama kuwapatia dhamana washtakiwa hao , kwani tayari wamefaata taratibu zote zinazotakiwa, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha hati ya kupinga kiapo hicho kilichowasilisha na mawakili wa Serikali, kilichopinga washtakiwa hao kupatiwa dhamana.

Hata hivyo baada ya upande wa Washtakiwa hao, kuwasilisha maombi hayo. Upande wa Mawakili wa Serikali nao waliendelea na msimamo wao, na kuiomba Mahakama izuie dhamana hiyo, hadi hapo nao watakapopitia hati iliyowasilisha na upande wa utetezi ya kutaka washtakiwa hao wapatiwe dhamana kwani ni haki yao ya msingi.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, Hakimu wa kesi hiyo Ivan Msaki alichukua maamuzi  ya kuhairisha  tena kesi hiyo hadi  Desemba 6 ya Mwaka huu, ambapo watakutana tena kujadili juu ya   kiapo  kilichokuwa kimewasilishwa na upande wa mawakili wa Serikali, kupinga washtakiwa hao kupatiwa dhamana.

MWISHO

No comments:

Post a Comment