Thursday, December 28, 2017

MAUTI ILIYOZIKWA ZAIDI YA MWEZI MMOJA ULIOPITA YAFUKULIWA KWA LENGO LA KUCHUNGUZWA

GAIRO,MOROGORO
NA, OMARY HUSSEIN

Huzuni na simanzi zimetawala kwa zaidi ya masaa nne kwa wakazi wa kijiji cha Kilimani kata ya Msingisi wilaya ya Gairo mkoani Morogoro baada ya familia ya watoto wanne wakiongozwa na mama yao mzazi kufika kijijini hapo na kufukua kaburi alipozikwa baba yao aliyezikwa miezi miwili iliyopita, wakidai kuwa na mashaka na kifo chake ikiwa ni sehemu moja wapo ya kutekeleza agizo la mahakama ya hakimu Mkazi mkoa wa  Morogoro.

Wanafamilia hao walifika kijijini hapo wakiwa na ulinzi wa polisi kwa ajili ya kusimamia kufukuliwa kwa kaburi hilo na watoto hao kupata nafasi ya kuhakikisha kama mwili uliozikwa ni baba yao mzazi au siyo pamoja na kufanyiwa uchunguzi kubaini sababu zilizopelekea kifo chake huku wakisema kilicho wasukuma kufika mahakamani ni kutokuwepo maelewano mazuri baina ya ndugu wa upande wa baba yao  kutokana na marehemu huyo kufariki na kuzikwa bila kupewa taarifa yoyote walisema watoto wa Marehemu Merina na Yared Stanford.
Baadhi ya watoto wa Marehemu wakitafakari baada ya kuona mwlili wa marehemu baba yao


Kwa mujibu wa Mke wa marehemu Julieth Majaliwa amesema mara ya mwisho kuwasiliana na mumewe walikua  nyumbani kwao jijini Dar es salaam ambapo alimuaga anaenda kijijini kwao kuwajulia hali ndugu zake  lakini tangu alivyo ondoka hawakuwa tena na mawasiliano nae mpaka waliposikia kwa watu kuwa mume wake amefariki dunia
Baadhi ya Familia wa Marehemu wakiangua kilio baada ya kuona mwili wa Marehemu

Mjomba wa Marehemu aliyefahamika kwa majina ya Mlinga Alpakshad amesema wameamua kumzika marehemu huyo bila kutoa taarifa kwa familia yake kutokana na watoto pamoja na mama yao   kumtelekeza wakati alipokuwa anaumwa.
 
Mwili wa Marehemu Stanford Gombo ukitolewa kaburini

Kwa mujibu wa daktari Msaidizi Mwandamizi George Mkoba kutoka hospitali ya wilaya ya gairo amesema kwa sasa wamechukua baadhi  vipimo (SAMPULI) kwa ajili ya kupelekwa kwa mkemia mkuu kwa ajili ya vipimo zaidi  kama walivyoagizwa na mahakama.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu Mzee Stanford Gombo amefariki dunia Novemba 11 mwaka huu kijijini hapo  baada ya kuugua kwa muda mrefu, huku familia yake ikiongozwa na Mama na watoto wa nne wakidai kutokuwa na taarifa ya kuugua kwake mpaka kufariki dunia, hatua iliyopelekea wao kukimbilia mahakamani.


MWISHO

No comments:

Post a Comment