
Kampuni hodhi ya rasilimali za reli nchini (Rahco) imeanza utekelezaji wa kubomoa nyumba zote zilizojengwa ndani ya njia ya reli katika mkoa wa Mwanza huku zaidi ya wafanyabiashara 200 wa samaki na dagaa jijini humo wakikosa sehemu ya kwenda kufanyia biashara zao baada ya kubomolewa vibanda vyao.
Hata hivyo, tofauti na vilio vya baadhi ya wananchi wengine wanaokumbwa na adha kama hiyo, baadhi ya wafanyabiashara hao walikiri kuvamia eneo hilo tangu mwaka 1994 baada ya reli hiyo kuacha kufanya kazi.
Ofisa Mfawidhi wa Rahco, Daimon Mwakaliki alisema ubomoaji huo ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kupisha ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge.
Bila kutaja idadi ya nyumba za watu, taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, kidini, shule na viwanja vya michezo, zitakazoathirika, Mwakaliki alisema utekelezaji huo umeanza ikiwa ni siku tatu tangu Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuagiza kuanza ubomoaji huo.
Alisema watakaobomolewa ni wale waliojenga ndani ya mita 15 kutoka stesheni ya reli hadi bandarini na kutoka njia kuu ya reli na kuendelea, itakuwa mita 30.
“Zoezi hili si la kushtukizwa kwani tulitoa notisi kwa watu wote waliovamia miezi sita iliyopita, baadhi yao walibomoa wenyewe lakini baadhi walikaidi ingawa pia juzi tulipita kwenye maeneo yote yatakayobomolewa kuwatangazia kuanza kuwabomolea,” alisema Mwakaliki.
Bomoabomoa hiyo imeukumba ukuta wa Uwanja wa Nyamagana, ukuta wa Mamalaka ya Bandari, kiwanda cha samaki cha Vicky na taasisi nyingine yakiwamo makanisa na nyumba za kawaida.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment