Polisi mkoani Mara inamshikilia mganga wa zahanati katika Kijiji cha Rwamchanga wilayani Serengeti kwa madai ya kushindwa kumhudumia mjamzito aliyejifungua pacha na kusababisha kifo cha mtoto mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhan Ng’anzi alisema tukio hilo lilitokea Mei 15 na mtuhumiwa amekamatwa kwa makosa matatu, likiwamo la uzembe, kufanya makusudi na kushindwa kuwajibika sawa na kiapo cha kazi yake, huku akisema wanaendelea na mahojiano yatakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Muuguzi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema walipopima uzito wa watoto kwa mjamzito huyo walibaini kuwa aliyefariki alikuwa na kilo 2.5 na mwingine 2.3.
Muuguzi wa zahanati hiyo, Frida Kasonga alisema aliposikia taarifa ya kuwepo kwa mgonjwa huyo alilazimika kurudi kituoni kumsaidia lakini alikuta mtoto mmoja ameshafariki dunia.
Ofisa mtendaji kata, Fadhila Nyamburapi na Mwenyekiti wa kitogoji cha Kazi, Samwel Nyakande walilaani kitendo hicho na kutaka sheria ichukue mkondo wake.

No comments:
Post a Comment