Wednesday, January 11, 2017

MBUNGE WA JIMBO LA KILOMBERO AHUKUMIWA MIEZI SITA JELA

Kilombero, Morogoro.


Mahakama ya Wilaya ya Kilombero imemuhukumu kifungo cha miezi Sita mbunge wa Jimbo Kilombero mkoani Morogoro kupitia chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema Peter Lijualikali wenye miaka (30) mara baada ya kumkuta na hatia ya kufanya fujo na kusababisha taharuki katika uchaguzi wa kumtafuta mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Machi Mosi mwaka 2016 mwaka wa jana.



Peter Lijualikali ambaye ni mbunge wa Jimbo la Kilombero pamoja na Stephano Mgata,wote wawili wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Kilombero, baada ya kudaiwa kutenda kosa hilo Machi mosi mwaka jana saa nne Asubuhi katika  eneo la Kibaoni katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, ambako kulikuwa na uchaguzi wa kumtafuta mwenyekiti wa Halmashauri  hiyo. 



Washtakiwa hao kwa pamoja walifanya fujo hizo kinyume na kifungu namba 89, kifungu kidogo cha kwanza B cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002. Awali washtakiwa hao kwa pamoja walikana mashtaka na hivyo kufanya kesi hiyo kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na upande wa mashtaka ukathibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka. 


Hakimu mkazi wa mahakama ya Wilaya ya Kilombero Timothy Lyon amesema mahakama hiyo imewatia hatiani kwa kosa hilo na kwa kuwa mshtakiwa wa kwanza Mbunge Lijualikali ambaye alikuwa na kesi tatu huko nyuma na kutiwa hatiani, basi anahukumiwa jela miezi sita kutokana na mahakama kuona kuwa ni mzoefu, huku mwenzake ndugu Mgata yeye akihukumiwa kifungo cha miezi sita nje, kutokana na kuoneka ni mara ya kwanza kuhukumiwa. 


Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo mbunge huyo amepelekwa kwenye gereza la Kilimo la Idete, ambako ndiko atatumikia kifungo chake cha miezi sita. 


MWISHO.

No comments:

Post a Comment